Sure boy Rasmi Atambulishwa Yanga Fc

Sure boy Rasmi Atambulishwa Yanga Fc 

YANGA kwa sasa imekuwa ikiupiga mwingi kwa soka la pasi nyingi na kufanya mashabiki wao kutamba.

Hata hivyo, ikiwa na utamu wake, fasta mabosi wao wamemshusha kiungo fundi kutoka Azam, Abubakar Salum ‘Sure Boy’, ambaye licha ya kuibua vita mpya ya namba, lakini anaenda kuiongezea utamu zaidi.

Mbali na kiungo huyo, pia Yanga imemnasa Dennis Nkame akitokea Biashara United.

Kutua kwa wachezaji hao kunaends kumpa ugumu Kocha Nasreddine Nabi, juu nani achomoke kwenye kikosi cha sasa, ila kazi ikiwa eneo la kiungo kwani kumejaa mafundi watupu.

Ujio wa Sure Boy unafanya eneo hilo la kuwa na nyota sita wanaomudu kucheza safu ya kiungo unalipa uhakika benchi la ufundi kutumia mifumo na mbinu tofauti uwanjani kulingana na ubora wa timu pinzani.

Nyota sita waliopo Yanga iliyoongezewa nguvu moja dirisha hili la usajili ni Fei Toto, Aucho, Yannick Bangala, Mukoko Tunombe, Zawadi Mauya na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.

Katika kundi hilo Bangala, Mukoko, Aucho na Mauya wanamudu kucheza vyema kama viungo wakabaji.

Lakini bado Fei Toto, Sure Boy, na Bangala ambaye ni kiraka wanaweza kucheza pia nafasi ya kiungo namba nane kutegemeana na mahitaji ya kiufundi ya mechi husika.

Endapo benchi la ufundi litatumia mfumo wa 4-4-2, maana yake wataanza viungo wawili tu kati ya sita, mmoja akicheza namba nane na mwingine sita.

Kama Nabi atatumia mfumo wa 4-2-3-1, maana yake watano kati ya sita wanaweza kuanza pamoja ambapo kutakuwa na viungo watatu wa juu wataokuwa na kazi ya kumlisha fowadi mmoja atakayesimama mbele au hata wenyewe kufunga mabao pamoja na viungo wawili watakaocheza mbele ya mstari wa mabeki mfumo ambao mara nyingi Kocha Nabi amekuwa akiutumia.

Kutokana na uwezo wa baadhi ya viungo hao kumudu kucheza nafasi tofauti uwanjani, hata mfumo wa 3-4-3 unaweza kuwapa nafasi ya kucheza kundi kubwa la viungo hao.

Usajili wa Sure Boy unaweza kuongeza kitu zaidi Yanga kwa kuipa faida ya kuwa na mpango mbadala wa kupika mashambulizi na mbinu za kusaka bao langoni mwa timu pinzani.

Uwezo wa Sure Boy wa kupiga pasi za juu kwenda kwa washambuliaji, unaweza kuinufaisha Yanga, hasa kwa mastraika Fiston Mayele na Makambo wanaotumika kwa sasa eneo hilo.

 

Post a Comment

0 Comments